Polisi wakamata magari 23 ya wizi

0
260

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata Mohamed Amani (45) maarufu Kiziwi mkazi wa Dar es Salaam na Mwanza, Salome Richard (32) maarufu Mama G mkazi wa Mwanza na wenzao wanane kwa tuhuma za wizi wa magari katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amesema mbali na kuwakamata watuhumiwa hao, polisi pia wamekamata magari 23 ya aina mbalimbali katika mikoa ya Mwanza, Iringa, Kilimanjaro, Kagera na Dar es Salaam.

Amesema baada ya polisi kuwahoji kwa kina watuhumiwa hao waliwaonesha yalipo magari hayo.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, upelelezi umebaini kuwa watuhumiwa hao kabla ya kuiba magari hayo huyavizia yakiwa yameegeshwa kwenye maegesho ya jumla, binafsi na majumbani na baadae huvunja vitasa vya milango upande wa dereva na kuwasha gari kwa kutumia funguo bandia na kuondoka nayo.

Aidha Watuhumiwa hao baada ya kuiba magari hayo hubandika namba za usajili na chasses za magari yaliyopata ajali na kuuzwa kama vyuma chakavu.

Baadhi ya magari hayo tayari yametambuliwa na wamiliki, na upelelezi unaendelea.