Shambulio jingine latokea Pulwama

0
849

Askari wanne wameuawa  katika jimbo la Kashmir upande wa India kufuatia mapigano yaliyozuka baina ya skari hao na Wanamgambo wanaodhaniwa kuwa ni wa kutoka nchini Pakistani.

Mapigano hayo yametokea katika eneo la Pulwama, mahali ambapo zaidi ya askari Arobaini wa India waliuawa wiki iliyopita katika shambulio la kujitoa muhanga.

Vikosi vya India vipo katika eneo hilo la Pulwama kwa ajili ya operesheni ya kuwasaka wanamgambo waliofanya shambulio hilo la wiki iliyopita.

Wakati hayo yakiendelea, Pakistani imemuita nyumbani Balozi wake nchini India kwa majadiliano zaidi, kufuatia kuwepo kwa  hali ya kutoelewana baina ya nchi hizo baada ya shambulio hilo la kujitoa muhanga.

Nayo India tayari imemuita nyumbani Balozi wake nchini Pakistani kufuatia hali inayoendelea hivi sasa,  ambapo pia nchi hiyo imeishutumu Pakistani kwa kutovichukulia hatua vikundi vya Wanamgambo ambavyo vimekua vikifanya mashambulio ya mara kwa mara katika jimbo hilo la Kashmir upande wa India.

Shambulio la kujitoa Muhanga lililotokea wiki iliyopita ambalo ni baya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 30 katika jimbo la Kashmir, lilitekelezwa na kijana  mwenye umri wa kati ya miaka 19 na 21.

Habari zaidi kutoka nchini India zinasema kuwa mshambuliaji huyo alitumia gari lililosheheni mabomu kugonga  basi lililobeba askari wa India waliokuwa wakienda doria.