Wizara ya Nishati imetangaza kuandaa kongamano la nishati safi ya kupikia ‘Clean Cooking Conference’ ili kuchunguza vikwazo vinayodumaza matumizi ya nishati za kisasa za kupikia na kupendekeza mikakati ya kufanikisha upatikanaji wa nishati safi, za bei nafuu na endelevu nchini Tanzania.
Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kuwa mkutano huo utakaofunguliwa na Rais Samia Suluhu utafanyika Novemba 1 na 2, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha watunga sera, wadau wa maendeleo, wajasiriamali, wawekezaji, wafadhili, wanataaluma na wananchi kwa ujumla.
Makamba amesema kuwa 90% ya nishati inayotumika kupikia nchini ni kuni na mkaa hali inayosababisha vifo vya Watanzania zaidi ya 33,000 kila mwaka kutokana na magonjwa yasababishwayo ni nishati chafu, wanawake na watoto wakiwa waathirika wakubwa.
Katika kongamano hilo, wataalamu kutoka sekta za umma na binafsi watajadili masuala mbalimbali kuhusu hali ya kupika nchini Tanzania; kubadilishana uzoefu kuhusu nishati safi za kupikia; kutathmini sera, sheria, udhibiti, uwezeshaji wa kifedha na teknolojia ili kukabiliana na changamoto. Kongamano linategemewa kujenga ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau.
“Tanzania kwa sasa ni moja ya nchi za chini kabisa duniani kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia tukiwa na kati ya 4-5% ya watu wanaitumia. Lengo letu ni kupandisha idadi hii hadi kufikia 80% katika miaka 10 ijayo. Lengo hili linawezekana kabisa na linafanyika,” amesema Makamba.