Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana, ametoa wito kwa watanzania kujifunza masuala ya uongozi kutoka kwenye urathi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Amesema hatua hiyo itawasaidia kufahamu namna ya kuishi na watu na kuwa viongozi bora.
Kinana ameyasema hayo Kibaha mkoani Pwani wakati wa mdahalo wa kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa Kushirikiana na Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere.
Amesema yapo mambo mengi ambayo Watanzania wanaweza kujifunza hasa kuhusu uongozi kutoka kwa Hayati Mwalimu Nyerere ambaye katika uhai wake alikuwa kiongozi muadilifu.
Ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitambua kuwa ili kuongoza vema Taifa lenye amani na uhuru, ni vema kuhakikisha Taifa hilo linazungukwa na majirani wenye amani na uhuru.
“Baba wa Taifa aliamini katika uhuru wa Bara la Afrika, alikuwa muumini mkubwa wa ukombozi wa Afrika.” amesema Kinana
Aidha, Makamu Mwenyekiti huyo wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara
amewasihi viongozi mbalimbali nchini kuepuka utukufu na kujali zaidi utumishi.