Mafunzo ya kuendeleza ujuzi yanayotolewa kupitia ruzuku ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), yametengeneza fursa za ajira kwa mamia ya vijana na akinamama wilayani Rungwe mkoani Mbeya kupitia mradi wa kufuga samaki.
Mkurugenzi wa shamba la kufugia samaki la RiverBanks Fish Farms ambalo ni miongoni mwa taasisi zilizofadhiriwa na SDF Pius Nyambancha
amesema hayo alipozungumza na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia, ambao ni wafadhili wa mradi huo, viongozi kutoka wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wale wa kutoka TEA.
Amesema ruzuku ya SDF imemwezesha kufuga samaki kitaalamu ikiwa ni pamoja na kumpa uwezo wa kuzalisha vifaranga, hivyo kumwongezea uzalishaji ambapo katika kipindi cha miezi tisa amezalisha kilo 600 za samaki.
Kupitia ruzuku ya SDF, kampuni ya RiverBanks Fish Farms ilipata ufadhili wa shilingi milioni 131.2, ambazo zimewezesha uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji vifaranga vya samaki, ufugaji wa kisasa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya ufugaji pamoja na kuendesha mafunzo kwa vijana na akina mama 427 na 7 kutengeneza ajira kwa watanzania 726.