Wadau wa utalii watakiwa kuhudhuria majukwaa mbalimbali

0
636

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wadau wa sekta ya utalii nchini kuhudhuria majukwaa mbalimbali katika mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheji ya Afrika unaoendelea jijjji Arusha, ili kujifunza na kuongeza ujuzi katika sekta ya utalii.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akifungua mkutano huo unaofanyika kwa muda wa siku tatu.

“Napenda kutoa rai kwa wadau wa utalii mtakaoshiriki tukio hilo muhimu hususani kutoka taasisi zinazohusika na usimamizi, utangazaji na usafirishaji wa vivutio vya utalii nchini kushiriki kikamilifu kwa lengo la kupata ujuzi utakosaidia kuendeleza sekta hiyo.” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa

Mkutano huo wa 65 wa UNWTO Kamisheni ya Afrika unafanyika kwa pamoja na matukio mbalimbali ya kimkakati likiwemo Jukwaa la Masoko (Digtal marketing), jukwaa linalotoa fursa kwa wataalam nguli wa masuala ya masoko katika sekta ya utalii kuwasilisha mada zinazohusu sekta hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya utalii.

Pia Waziri Mkuu amesema mkutano wa 65 wa UNWTO ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026, ambao umeainisha utalii wa mikutano na matukio kama zao la utalii na kimkakati katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania.