Serikali : Mkutano wa UNWTO ni matokeo ya amani

0
685

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana amesema, Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO)
Kamisheni ya Afrika ni matunda ya amani na utulivu uliopo nchini pamoja na uwepo wa miundombinu mizuri ya usafiri.

Dkt. Chana ameyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Arusha, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

“Mkutano huu ni matokeo ya amani na utulivu, amani ambayo imekuwepo nchini kwetu tangu uhuru sanjari na maendeleo ya miundombinu muhimu ya usafiri ambayo imevutia kufanyika kwa mkutano huu.” amesema Balozi Pindi Chana

Mkutano huo wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani
Kamisheni ya Afrika unafanyika kwa muda wa siku tatu na unahudhuriwa na washiriki kutoka nchi 33, wadau wa utalii pamoja na Mawaziri wa Utalii kutoka katika nchi hizo 33.

UNWTO ilianzishwa mwaka 1946 ikiwa chini ya Umoja wa Mataifa, na lengo la uanzishwaji wake lilikuwa ni kutangaza utalii unaowajibika, endelevu na unaofikiwa na watu wote.

Mpaka sasa ina wanachama 160, ambapo Tanzania ni moja ya wanachama waanzilishi.