Bunifu za kiteknolojia kwenye afya kuenea nchi nzima

0
288

Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kukuza teknolojia zitakazosaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo huko Doha, Qatar wakati wa ufunguzi wa mkutano wa dunia katika ubunifu wa masuala ya afya (WISH 2022), mkutano unaohudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa masuala ya afya.

Amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa, zipo bunifu mbalimbali za kidijitali zinazotumika katika sekta ya afya nchini na zimeonesha matokeo chanya.

“Kama nchi nyingine yoyote ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania imetumia fursa ya ukuaji wa haraka wa teknolojia ya kidijitali kwa njia ya simu kuanzisha afua mbalimbali za kibunifu kama vile jukwaa la simu la M – MAMA linalowaunganisha wajawazito na usafiri wa dharura kwenda kwenye vituo salama vya afya.” amesema Rais Samia

Aidha, Rais Samia amesema kutokana na bunifu hizo kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja mfano M – MAMA na ubunifu wa kutengeneza mashine za kuhifadhia watoto wachanga zinazotembea kutoka eneo moja hadi jingine, kwa sasa zitasambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.