Maagizo matatu ya Rais kwa Mawaziri

0
277

Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza mawaziri ambao amekuwa akiwateua kutekeleza majukumu yao huku wakizingatia mambo makubwa matatu.

Mambo hayo ni kuheshimu katiba ya nchi, kufahamu mipaka yao na kuwa na siri.

Rais Samia ameyasema hayo Ikulu mkoani Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri watatu kufuatia mabadiliko madogo aliyoyayafanya katika Baraza la Mawaziri hapo jana.

Amesema kwa Mawaziri ni muhimu kuheshimu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kutoa maamuzi ya mambo mbalimbali, kwani bila kufanya hivyo watakua wanakiuka baadhi ya mambo.

Pia amesema lazima wajue mipaka yao iwe ni kwenda juu au chini, jambo linatalosaidia kutoa maamuzi ambayo wakati mwingine hawastahili kuyatoa.

Jambo lingine ambalo Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ni Mawaziri kuwa na siri, hasa mambo yanayojadiliwa ndani ya serikali na kwenye Baraza la Mawaziri.

Mawaziri walioapishwa hii leo na Rais
Samia Suluhu Hassan ni Angellah Kairuki ambaye ameapishwa kuwa waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Wengine ni
Dkt. Stergomena Tax ambaye ameapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Innocent Bashungwa aliyeapishwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.