Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa Watanzania kutoa maoni kuhusu maboresho ya sheria mpya ya uwekezaji
ambayo ilisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa nane wa Bunge.
Amesema sheria hiyo sasa imepelekwa kwa wananchi ili nao watoe maoni yao ya kuiboresha, lengo likiwa ni kuifanya ifae kutumika kwa maendeleo ya Taifa.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizindua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji linalounganisha wafanyabiashara wa Tanzania na Italia.
Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwa dhati kuwalea vema wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, ndio maana amepunguza kiasi cha fedha alichotakiwa kuwa nacho mwekezaji ili aweze kujisajili katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Waziri huyo wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara amesema
awali mwekezaji alitakiwa kuwa na dola laki moja za kimarekani ili ajisajili, ila sasa atapaswa kuwa na dola elfu hamsini tu.
Amesema kutokana na juhudi za serikali katika kuimarisha diplomasia ya kiuchumi baina ya Tanzania na mataifa ya nje, kumekuwa na matokeo chanya katika sekta ya biashara ambapo hivi sasa kampuni za uwekezaji takribani 40 kutoka Italia zimeshiriki katika jukwaa hilo la Biashara na Uwekezaji linalounganisha wafanyabiashara wa Tanzania na Italia.
Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, hadi sasa uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni mbili za kimarekani umeshafanyika hapa nchini kutoka kwa kampuni za nchini Italia.