EAAW yatoa chanjo kwa mbwa Mkalama

0
169

Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na ustawi wa Wanyama nchini (EAAW) limetoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa, kwa mbwa zaidi ya 500 na paka 29 wilayani Mkalama mkoani Singida.

Mkurungenzi wa Shirika hilo Ayubu Nnko amesema, chanjo hiyo imetolewa wakati wa wiki ya maadhimisho ya kichaa cha Mbwa duniani, ambayo huadhimishwa Septemba 28 ya kila mwaka.

Amesema chanjo hiyo ilianza kutolewa tarehe 23 mwezi huu na itaendelea kutolewa hadi Oktoba mbili mwaka huu.

Nnko ameongeza kuwa kwa muda mrefu EAAW imekuwa ikishirikiana na uongozi wa wilaya ya Mkalama katika kutoa chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa pamoja na matibabu, lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Kwa upande wake daktari wa Mifugo wa wilaya ya Mkalama, Elias Mbwambo amelishukuru shirika hilo lisilo la kiserikali linalojihusisha na ustawi wa Wanyama nchini,c na kusema kuwa limekuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Ameitaka jamii kutoa ushirikiano katika matunzo ya mbwa na paka, ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea na wafugaji kuhakikisha mbwa wanaofungwa kwenye banda au mnyororo wamepata chanjo.