Majaliwa awasilisha salamu za pole Japan

0
295

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida na kuwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kifo cha Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo Shinzo Abe.

Katika mazungumzo hayo mbali na Waziri Mkuu Majaliwa kutoa pole, ametumia fursa hiyo kusisitiza kuimarishwa kwa uhusiano baina ya Tanzania na Japan.

Pia Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kukumbushia masuala ambayo walijadiliana kwa njia ya mtandao wakati akiwa Tunisia kwenye mkutano wa TICAD 8 hasa utekelezaji wa miradi ya zamani ambayo Tanzania iliiwasilisha kwenye mkutano wa TICAD 7, inayohusisha ujenzi wa bandari ya Kigoma, mradi wa maji wa Zanzibar na ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha hadi Holili mkoani Kilimanjaro.

“Nimemshukuru Waziri Mkuu wa Japan kwa ahadi yake kuwa wanafuatilia pia maombi ya miradi nane ambayo tuliiwasilisha kwenye mkutano wa TICAD 8 na majadiliano yameanza huko nyumbani.” amesema Waziri Mkuu

Miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa barabara ya Morogoro – Dodoma kwa kiwango cha lami, mradi wa umwagiliaji katika bonde la ziwa Victoria, mradi wa kusambaza maji Lugoda (Mufindi), kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam, bandari ya kisasa ya uvuvi, kuanzisha maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi na ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amesema watatekeleza ahadi yao ya kuzisaidia nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo ili zijitegemee kwa chakula.

Amesema kupitia benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Japan itatoa dola milioni 300 za Kimarekani, ili kuzisaidia nchi za Afrika zizalishe chakula kwa wingi na kukabiliana na upungufu wa chakula uliojitokeza baada ya kuzuka kwa vita baina ya Russia na Ukraine.