TRA yapendekeza uwepo somo la kodi shuleni

0
293

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imependekeza kuingizwa kwa elimu ya kodi katika mitaala ya elimu nchini Tanzania kuanzia kwenye Shule za Msingi hadi Sekondari.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo amesema Mamlaka hiyo inaamini kwamba kama kungekuwa na somo la kodi linalosomwa na Wanafunzi wote katika shule za Msingi na Sekondari basi Taifa lingeweza kuwa na raia wengi wanaoelewa kuhusu kodi.

Amesema TRA inakusanya kodi kutoka kwa Walipa kodi wengi ambao hawana ufahamu au hawajui umuhimu wa kulipa kodi hivyo kama Wanafunzi watafundishwa somo la kodi Shuleni itasaidia kupata Raia wenye uelewa mpana kuhusu kodi na kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari.

Baada ya TRA kuwasilisha maoni hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uboreshaji wa Mitaala, Profesa Maboko amewashukuru kwa mapendekezo waliyoyatoa na kuahidi kuyafanyia kazi katika maboresho ya Mtaala wa Elimu yanayoendelea kufanywa nchini Tanzania.