Tanzania yasisitiza mazungumzo kutatua migogoro

0
186

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania bado inaamini kuwa diplomasia na mazungumzo ndio chombo bora cha kutatua migogoro duniani.

https://www.youtube.com/watch?v=LzEl4aBSJss&t=2s

Amesema ni muhimu kushiriki katika kutafuta utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani, ili kukabiliana na athari zitokanazo na migogoro hiyo kama vile ongezeko la bei za vyakula na mafuta pamoja na kushuka kwa uzalishaji katika sekta za kilimo na viwanda duniani kote.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA), unaondelea jijini New York nchini Marekani.

Amesema licha ya migogoro iliyopo duniani, mataifa yanapaswa kulinda maisha ya binadamu hasa watoto na wanawake pamoja na ustawi wa watu wote.

Makamu wa Rais amesema katika kulinda amani, Tanzania inajivunia kuchangia askari katika misheni tano kati ya 16 zilizopo za kulinda amani duniani kote, na kwamba Taifa lipo tayari kuchangia zaidi iwapo litaombwa kufanya hivyo.

Ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuongeza uungaji mkono wake kwa juhudi za kikanda za kujenga na kulinda amani.

Dkt. Mpango pia amepongeza juhudi za Umoja wa Mataifa katika kukuza lugha ikiwemo tamko la kihistoria la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lililoitaja Julai 7 ya kila mwaka kuwa ni Siku ya lugha ya Kiswahili Duniani.

Dkt. Mpango amehutubia mkutano huo wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.