Wawakilishi 9 wa EALA wapatikana

0
119

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limewachagua wawakilishi tisa kwenye Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwezi Desemba mwaka huu.

Akitangaza majina ya washindi wa uchaguzi wa wawakilishi hao, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amewataja kuwa ni pamoja na Angela Kizigha ambaye ameshinda kwa kipindi cha pili, Nadra Juma Mohamed na Dkt. Shogo Mulozi.

Wengine waliochaguliwa ni Abdulla Hasnuu Makame ambaye amechaguliwa kwa kipindi cha pili, Machano Ally Machano na Aswar Kachwamba.

Wawakilishi wengine ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Simanjiro James Ole Millya, Dkt. Ng’waru Maghembe huku nafasi ya uwakilishi kwa walio wachache ikichukuliwa na Mgombea wa Chama Cha Wananchi (CUF) Mashaka Khalfan Ngole.

Mara baada ya kutangaza matokeo hayo Spika wa Bunge akawataka wawakilishi hao kuhakikisha wanatanguliza maslahi ya Taifa mbele na wasiende na mawazo yao binafsi bali falsafa za watanzania katika kukitumikia chombo hicho.