Majaliwa ataka viashiria vya uvunjifu wa amani vidhibitiwe

0
699

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji wote wa serikali kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Amesema lengo la agizo hilo ni kusisitiza utekelezwaji wa maono na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Kilimanjaro wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.

Amesema Watanzania hawana budi kuitunza amani kutokana na umuhimu wake, na kuongeza kuwa amani ni tunda la upendo, utulivu, mshikamano na maridhiano.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwa upande wa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kikanda na za kimataifa, katika kutafuta na kudumisha amani na usalama.

Pia amesema serikali itaendelea kuchukua hatua na tahadhari zote zinazohitajika, ili kuendelea kudumisha amani nchini kote.

“Serikali ya awamu ya sita inafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa kwa kuweka mikakati mbalimbali ya maendeleo inayolenga kutokomeza umaskini, umaskini ni chanzo kikubwa cha migogoro sehemu nyingi duniani kwa sababu watu wanagombania kufaidika na rasilimali chache zilizopo.” amesema Waziri Mkuu