Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula amezindua mkakati wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi katika Kanda ya Ziwa.
Dkt Mabula amefanya uzinduzi huo jijini Mwanza alipokutana na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za jiji hilo na wilaya ya Ilemela.
Akizindua mkakati huo wa ukusanyaji kodi ya Pango la Ardhi katika Kanda ya Ziwa, Naibu Waziri Mabula amesema kuwa mkakati huo si kwa Kanda ya Ziwa pekee bali utakua kwa nchi nzima ambapo wadaiwa wote sugu wa kodi hiyo watafikishwa katika Mabaraza ya Ardhi.
Ametolea mfano jiji la Mwanza ambalo hadi kufikia Januari 30 mwaka huu limekusanya jumla ya Shilingi Bilioni Tatu Nukta Nne kati ya Shilingi Bilioni Saba Nukta Nne zilizotakiwa kukusanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Ili kuhakikisha halmashauri zote zilizopo katika Kanda ya Ziwa zinakusanya kodi ya Pango la Ardhi kwa mafanikio, Naibu Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameiagiza Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa, kuwafikisha wadaiwa wote katika mabaraza ya ardhi bila kujali kama ni taasisi za umma au la.