Polisi : Barabara ya mwendokasi marufuku

0
185

Jeshi la Polisi nchini limerudia kusisitiza kuwa ni marufuku kwa chombo chochote cha moto zikiwemo baiskeli, pikipiki na guta kupita katika barabara ya mwendokasi zaidi ya mabasi yaendayo kwa haraka.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime ametoa kauli hiyo kufuatia kusambaa kwa video fupi katika mitandao ya kijamii ikionesha mzozo kati ya walinzi/wafanyakazi wa barabara hiyo na askari polisi waliokuwa wakilazimisha kupita kwenye barabara hiyo.

Amesema raia yeyote na wa cheo chochote awe anaendesha chombo cha moto au awe anaendeshwa, ni marufuku kupita katika barabara hiyo.

Jeshi la Polisi nchini limeonya kuwa, mtu yoyote atakayepita ama kulazimisha kupita kwenye barabara hiyo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kujulisha mamlaka anayotoka kama ni mtumishi wa umma, ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake.