Tanzania Yang’ara tamasha la JAMAFEST

0
1509

Tamasha la Tano la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Sanaa na Utamaduni (JAMAFEST) limefungwa rasmi Bujumbura nchini Burundi kwa Burundi kukabidhi Bendera ya Jumuiya hiyo kwa Sekretarieti hadi itakapotangazwa nchi ambayo itakuwa mwenyeji wa tamasha la sita.

Katika Tamasha hilo, Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika Sanaa za Jukwaani ambapo Septemba 9, 2022 Muziki wa taarabu umepeperusha vyema bendera ya Taifa kupitia kikundi cha Taifa cha Taarabu Asilia kutoka Zanzibar huku wasanii nguli wa muziki huo Abdul Misambano na Mzee Yusufu wakiibua shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi wa Burundi waliofurika katika viwanja vya Intwari jijini Bujumbura.

Akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika Tamasha hilo, Mratibu wa JAMAFEST Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Leah Kihimbi amesema Tanzania imefanya vizuri kwa kuwaleta wasanii wengi kwa fani mbalimbali ikiwemo taarabu, muziki wa Singeli na  ngoma za asili.

Akifunga tamasha hilo, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki, Vijana, Michezo na Utamaduni Burundi Severin Mbarubukeye amesema kuwa amefurahishwa kwa ushiriki wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye Tamasha la Tano JAMAFEST nchini humo.