Mazingira ya Uwekezaji kuendelea kuboreshwa

0
830

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, -Angellah Kairuki amesema kuwa serikali imeweka mpango wa kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kurahisisha upatikanaji wa vibali kwa wawekezaji na ardhi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na maeneo ya kilimo.

Waziri Kairuki ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari baada ya kupokea ujumbe wa Wafanyabiashara Saba wa Hongkong  – China ambao wapo nchini kwa lengo la kufanya utafiti wa maeneo ya uwekezaji wakiwawakilisha wafanyabiashara wa nchi hiyo.

Amesema kuwa hivi sasa wizara yake iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,  imeanza kuufanyia kazi mpango huo ambapo pamoja na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuingiza fedha za kigeni pia utaongeza ajira kwa watanzania.

“Sisi kama serikali lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaimarisha uwekezaji, mpango huo ambao ulifanyika mwezi Mei mwaka 2018 unalenga kuondokana na vikwazo vya kibiashara na kuharakisha vibali na kutoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji, tunayafanya haya ili kuongeza ufanisi katika sekta ya uwekezaji, tunataka Watanzania wanufaike” amesema Waziri Kairuki.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Balozi wa Heshima wa Tanzania huko Hongkong, -Jessica So  amesema kuwa lengo la safari yao ni kufanya utafiti wa maeneo ya uwekezaji na  biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), -Geoffrey Mwambe amesema kuwa tayari kituo hicho kimefanya mazungumzo na  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Hongkong ambayo inashughulikia Biashara na Uwekezaji, mazungumzo yatakayowezesha kusainiwa kwa makubaliano yenye lengo la  kuhakikisha wafanyabiashara wengi wanatumia fursa zilizopo Hongkong na Tanzania.