Kampuni ya Apple imeachilia sokoni bidhaa yake mpya ya Apple Watch Series 8, ambayo ina vipengele vipya vya kutambua ajali ya gari pamoja na hali ya afya ya uzazi kwa wanawake.
Hata hivyo toleo hilo la saa kupitia kipengele cha ufuatiliaji wa afya ya uzazi kwa wanawake limeibua wasiwasi na hisia tofauti kwa raia wa Marekani, kutokana na kuwepo kwa sheria mpya nchini humo inayodhibiti suala la utoaji mimba.
Wasiwasi ni kwamba data kuhusu mzunguko wa hedhi zinaweza kutumiwa na vyombo vya sheria nchini humo katika uchunguzi.
Kampuni hiyo ya Apple kupitia kwa Afisa Mkuu wake wa uendeshaji Jeff Williams, imewatoa hofu wale wote wenye wasiwasi huo na kueleza kuwa data zote kutoka kwenye vifaa vya Apple zinalindwa kwa umakini na zinaweza kupatikana tu kupitia nywila na alama za vidole yaani “biometric” kutoka kwa mtumiaji.
Kwa upande wa kipengele kipya cha utambuzi wa ajali ya gari, kwa kutumia vitambuzi saa hiyo itaweza kutambua ajali mbaya na pale inapokuwa imetokea itaunganisha moja kwa moja taarifa za ajali za mtumiaji wa saa hiyo na huduma za dharura zinazopatikana katikamazingira ya karibu na eneo la ajali.