CCM yatoa neno kuhusu tozo

0
131

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeishauri serikali kutazama upya tozo mbalimbali wanazotozwa wananchi, ili kuwaletea unafuu tofauti na ilivyo sasa ambapo tozo hizo zimeonekana kuwa ni mzigo kwao.

Ushauri huo umetolewa na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya CCM Lumumba mkoani Dar es Salaam.

Shaka amesema wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya CCM waliokutana Septemba 6, 2022, wamejadili na kuishauri serikali kuangalia vyanzo vingine vya kupata fedha Ili kupunguza tozo kwa wananchi.

Amekiri suala la tozo kuwa na changamoto kadhaa ambazo hata hivyo zinaweza kushughulikiwa, na hivyo kuwataka watanzania kuwa watukivu wakati jambo hilo linashughulikiwa.

Shaka ameongeza kuwa serikali inayoongozwa na ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inashughulikia changamoto zilizojitokeza katika tozo.

“Tuendelee kuwa wazalendo maana dhamira ya Serikali ni njema na Rais ni msikivu na anashaurika na anasikiliza vilio vya wananchi hadi wa chini kabisa, maana hakuna mafanikio yasiyo na changamoto na hakuna changamoto isiyokuwa na mafanikio, tuzidi kumuamini Rais Samia maana Mungu amempa upeo na anajua watanzania wanataka nini.” ameongeza Shaka

Aidha amesema, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM imeazimia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa Taifa pamoja na kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agosti 23 mwaka huu.

Pia imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kwa kusimamia vizuri utendaji kazi wa serikali na kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.