Russia ina mpango wa kuzima mtandao wa Intaneti kwa muda na hivyo kujitoa kwenye mawasiliano na dunia.
Hatua hiyo itafanya mawasiliano baina ya raia na mashirika ya Russia kubaki ndani ya nchi hiyo badala ya kupitia njia za kawaida za Kimtandao wa Kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Russia imesema kuwa mpango huo wa kujitoa kwenye mawasiliano na dunia kwa muda ni jaribio la nchi hiyo la kujikinga dhidi ya mashambulio ya Kimtandao.
Jaribio la kuzima mtandao huo wa Intaneti linatarajiwa kufanyika kabla ya tarehe Mosi mwezi Aprili mwaka huu, lakini hata hivyo siku rasmi ya kuzimwa kwa mtandao huo haijatajwa.
Muswada wa sheria wa kuruhusu mabadiliko ya kiufundi ili Russia iweze kuendesha mtandao wake wenyewe wa Intaneti uliwasilishwa katika Bunge la nchi hiyo mwaka 2018.
Muswada huo pamoja na mambo mengine, unawataka watoa huduma za Intaneti nchini Russia kuwa na uwezo wa kuendelea na huduma zao hata pale ikitokea nchi za kigeni zikiamua kuitenga nchi hiyo.
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) na washirika wake wamekuwa wakitishia kuiwekea vikwazo vya kimtandao Russia kwa madai kuwa nchi hiyo imekua ikifanya mashambulio ya kimtandao.
Ili kujilinda na tishio hilo, Russia imeamua kutengeneza mfumo wake binafsi wa anuani za kimtandao ili iweze kupata mawasiliano hata pale itakapowekewa vikwazo hivyo ama itakapojitenga.