Liz Truss Waziri Mkuu mteule Uingereza

0
517

Chama tawala nchini Uingereza cha Conservative, kimemtangaza Liz Truss mwenye umri wa miaka 47 kuwa kiongozi mpya wa chama hicho na ambaye pia atachukua wadhifa wa Waziri Mkuu, kumrithi Boris Johnson aliyejiuzulu takribani miezi miwili iliyopita.

Liz Truss ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza na Rishi Sunak ambaye ni Waziri wa zamani wa Fedha, ndio walikuwa wakichuana vikali katika kinyang’anyiro hicho.

Katika kipindi cha takribani wiki nane, wanasiasa hao wamezunguka nchi nzima kuomba kura za wanachama, wakiahidi kushughulikia matazizo makubwa ya kiuchumi yanayoikabili Uingereza ikiwemo kupanda kwa bei ya nishati.

Katika kura zilizopigwa Liz Truss amepata asilimia 57 na mpinzani wake
Rishi Sunak amepata asilimia 43.

Anatarajiwa kuanza rasmi kutekeleza majukumu hayo ya Uwaziri Mkuu hapo kesho, baada ya kuidhinishwa rasmi na Malikia.

Liz Truss atakuwa Waziri Mkuu wa tatu mwanamke nchini Uingereza.