Mnadhimu mkuu JWTZ atembela Afrika ya Kati

0
426

Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jenerali Salum Haji Othman amefanya ziara maalum katika Kikosi cha walinda amani kutoka Tanzania kinachohudumu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Luteni Jenerali Salum Othman akiwa na ujumbe wake wamewasili katika uwanja wa ndege wa Berberati uliopo katika mkoa wa Mambere Kadei na kupokelewa na mwenyeji wake Kamanda Kikosi TANBAT 05 Luteni Kanali Adam Hamis Kiza, Maafisa na Askari mbalimbali wanaohudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa, MINUSCA katika Jamhuri ya Afrika ya kati.

Luteni Jenerali Othman amepokelewa na gwaride la heshma lililoandaliwa na TANZBAT 5 na baadae kupokea taarifa ya utendaji kazi ya Kikosi Kutoka kwa Afisa Mkuu wa Operesheni Meja Amulike Kabale.

Pamoja na mambo mengine Luteni Jenerali Salum Othman amepata wasaa wa kufanya mazungumzo na Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Amani – MINUSCA Luteni Jenerali Sidiki Traole yanayolenga utendaji kazi wa Kikundi cha walinda amani wa Tanzania.

Aidha, amepata fursa ya kufanya mazungumzo na maafisa na askari katika ukumbi wa Serengeti ambapo walinda amani hao walionyesha ari, hamasa na utayari wa kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani huku wakifata sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa, pamoja na za nchi husika.