Mwamuzi wa kati aliyesimamia mchezo baina ya Coastal Union na Young Africans SC, Raphael Ikambi kutoka mkoani Morogoro ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitatu baada ya kutenda kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Ikambi alishindwa kufanya maamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu katika tukio ambalo mchezaji wa Coastal Union, Mtenje Albano alimchezea mchezo hatarishi na usio wa kiungwana mchezaji wa Young Africans, Yanick Bangala ambaye baada ya tukio hilo aliinuka na kwenda kumsukuma Mtenje Albano.
Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 42:1(1.1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi. Yanga SC ilifanikiwa kuondoka na ushindi wa goli 0-2 dhidi ya wenyeji wa mchezo Coastal Union.