Rais Samia awataka Majaji kusimamia haki

0
232

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Majaji nchini kusimamia haki wakati wakitekeleza majukumu yao.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, mara baada ya kumuapisha Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza Mzee Ramadhan Nyamka pamoja na Majaji 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Amesema kilio kikubwa cha wananchi ni haki, hivyo ni vema kwa Majaji wa Makahama Kuu kuwa mfano kwa kutoa maamuzi yao huku wakisimamia haki.

Rais Samia ameongeza kuwa, katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha anashughulikia changamoto zinazowakabili Majaji ikiwa ni pamoja na kuteua Majaji zaidi kwa kuzingatia katiba ya nchi pamoja na uchumi unavyoruhusu.

Hafla ya kuwaapisha Majaji hao 21 wa Mahakama Kuu pamoja na
Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni pamoja na Wakuu mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.