Mrema kuzikwa alasiri Kiraracha

0
149

Mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha TLP Augustino Mrema yanafanyika leo alasiri nyumbani kwake katika kijiji cha Kiraracha, Vunjo mkoani Kilimanjaro.

Habari kutoka mkoani Kilimanjaro zinaeleza kuwa kwa sasa shughuli za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu Mrema, huku viongozi mbalimbali wa serikali, kisiasa na wastaafu wakishiriki katika shughuli hiyo.

Katika mazishi hayo ya Mwanasiasa huyo Mkongwe nchini, serikali inawakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene.

Miongoni mwa watu wanaoshiriki katika mazishi ya Mrema ni Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi,
James Mbatia.

Mrema alifariki dunia tarehe 21 mwezi huu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili mkoani Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.