Bilioni 1.2 Serengeti Girls, Tembo Warriors

0
255

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa amechangisha zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuchangia timu za Serengeti Girls na Tembo Warriors.

Harambee hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka timu hizo zichangiwe na wadau baada ya kufuzu kuingia kwenye mashindano ya kimataifa.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo lililofanyika mkoani Dar es Salaam Waziri Mkuu Majaliwa ameipongeza wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu, usimamizi na kutangaza shughuli za michezo kimkakati.

Aidha, amewapongeza wadau wote waliochangia ambapo amesema wameonesha uzalendo na kuwa sehemu ya kuzifanya timu hizo kushinda kwenye mashindano hayo.

Katika tukio hilo mbali na kupatikana kwa ahadi ya fedha hizo, wadau wametoa tiketi za wachezaji kwenda kwenye mashindano hayo na kurejea nchini, bima za afya kwa wachezaji wakiwa katika mashindano hayo na vifaa mbalimbali vya wanamichezo.

Kwa upande wake, waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa za kuongeza bajeti ya kuhudumia timu za Taifa, ukarabati wa viwanja na kuanzisha shule maalum za michezo ili kuvumbua na kuendeleza vipaji na hatimaye kupata timu bora za Taifa.