Zoezi la Sensa linaendelea

0
156

Zoezi la sensa ya watu na makazi linaendelea asubuhi hii baada ya kuanza saa sita na dakika moja usiku wa kuamkia hii leo katika maeneo mbalimbali nchini.

Maeneo ambayo zoezi la sensa lilianza usiku ni pamoja na kwenye vituo vya mabasi, viwanja vya ndege, mahospitalini na kwenye makazi yasiyo rasmi.

Kama ilivyokuwa kwa sensa nyingine zilizopita ambazo hufanyika kila baada ya kipindi cha miaka kumi, matokeo yake yatatoa takwimu za idadi ya watu zitakazoisaidia serikali kuandaa mipango ya maendeleo kwa wananchi wake kulingana na idadi ya watu.

Katika zoezi la sensa mwaka huu kuna moduli mbalimbali ambazo zinatumika kukusanya taarifa za watu na makazi yao nchi nzima.

Miongini mwa maswali yanayoulizwa ni yale yanayohusu taarifa za kidemografia,
maswali kuhusu umiliki wa nyaraka za kitaifa, taarifa za uzazi na vifo vilivyotokea ndani ya kaya na maswali ya kilimo na mifugo.

Tofauti ya sensa ya mwaka 2022 na sensa zilizopita kuna vitu vipya kama vile matumizi ya vishikwambi (tablets) katika hatua zote za utekelezaji wa sensa kwa lengo la kupunguza gharama.

Hii ni sensa ya sita tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26 mwaka 1964.

Sensa ya mwisho ilifanyika nchini mwaka 2012 ambapo takwimu zilionyesha Tanzania ina takribani watu milioni 45.