Raila atinga rasmi mahakamani

0
212

Mgombea wa kiti cha Urais nchini Kenya katika uchaguzi mkuu uliopita kupitia muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, leo amewasilisha rasmi ombi la kupinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi William Ruto kutoka muungano wa Kenya Kwanza.

Kesi hiyo imewasilishwa na mawakili wa Raila wakiongozwa na James Orengo.

Sheria kuhusu kesi ya kupinga matokeo ya Urais nchini Kenya inaeleza kuwa, iwapo kesi itawasilishwa siku ya mwisho ya muda uliowekwa, basi lazima ifanyike kabla ya saa nane mchana katika siku hiyo.

Kwa mujibu wa wakili wa muungano wa Azimio la Umoja Daniel Maanzo , kikosi cha mawakili kutoka muungano wa Azimio la Umoja tayari kimewasilisha kesi hiyo mtandaoni na kwamba watawasilisha stakabadhi zinazohitajika mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Baada ya kuwasilisha kesi hiyo mahakamani, muungano wa Azimio la Umoja una hadi tarehe 23 mwezi huu kukikabidhi chama cha UDA, Rais Mteule na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) malalamiko yao.