Serikali imetoa taarifa rasmi Bungeni jijini Dodoma kuhusu matukio ya mauaji na utekaji nyara watoto mkoani Njombe ambapo hadi hivi sasa watoto kadhaa wameuawa.
Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, -Kangi Lugola amesema kuwa tayari serikali imetuma makachero maalumu mkoani Njombe kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa matukio hayo.
Amesema kuwa mpaka sasa watu Ishirini na Tisa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Waziri Lugola ameliambia Bunge kuwa, serikali inasikitishwa na matukio hayo ya mauaji na itahakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi, – Kangi Lugola pia ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Njombe na Watanzania wote, kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola ili kukomesha vitendo hivyo vya mauaji ya watoto mkoani Njombe.