Tshisekedi aunguruma SADC

0
171

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri wa Kidemokrasi ya Congo amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kushirikiana katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya SADC, likiwemo lile la kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Rais Tshisekedi ametoa kauli hiyo katika mji mkuu wa DRC – Kinshasa, wakati wa mkutano wa 42 wa kawaida wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Uenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais Lazarus Chakwera wa Malawi Rais Tshisekedi amesema, katika kipindi chake atahakikisha mageuzi ya kiuchumi yanafanyika kwenye nchi wanachama wa SADC kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda na matumizi ya TEHAMA.

Awali akifungua mkutano huo wa
42 wa kawaida wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo aliyemaliza muda wake Rais Lazarus Chakwera amezitaka nchi wanachama kuzingatia misingi ya demokrasia ili kufanya ukanda huo kuwa sehemu salama kwa uwekezaji.

Tukio jingine muhimu lliloshuhudiwa wakati wa mkutano huo ni utolewaji wa medali za heshima kwa waanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, akiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, medali iliyopokelewa na mtoto wake Madaraka Nyerere.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi mbalimbali wanachama wa Jumuiya ya SADC akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Rais Philipe Nyusi wa Msumbiji.