Watendaji wa sekta ya sheria watakiwa kutenda haki

0
1011

Rais John Magufuli amewataka Watendaji wa sekta ya sheria nchini kuendelea kufanyakazi kwa uaminifu na haki licha ya changamoto mbalimbali zilizopo.

Rais Magufuli ametoa wito huo jijini Dar es salaam wakati wa kilele cha maadhimisho siku ya sheria nchini, maadhimisho yanayoashiria kuanza kwa shughuli za Kimahakama kwa mwaka huu.

Amesema kuwa kuna baadhi ya Watendaji wa sekta ya sheria nchini si waaminifu na wamekua hawatendi haki wakati wa kutoa maamuzi mbalimbali na hivyo kuwakoseha Watanzania haki yao ya kupata huduma za kisheria.

Amewataka Watendaji hao kuepuka upendeleo wakati wa kutoa maamuzi na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika shughuli zao za kila siku.

Kuhusu upungufu wa Watendaji wa sekta ya sheria nchini, Rais Magufuli amesema kuwa tatizo hilo ni kwa sekta zote, hivyo iwekwe mikakati ya kutumia waliopo hadi hapo bajeti itakaporuhusu.

Ameipongeza idara ya Mahakama nchini kwa mafanikio mbalimbali hasa katika kupunguza mrundikano wa kesi na kuongeza mapato baada ya kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato hayo.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma amesema kuwa Idara ya Mahakama imeendelea kupunguza mrundikano wa kesi katika mahakama mbalimbali nchini.

Profesa Juma amesema kuwa mrundikano huo wa kesi umepungua zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo kesi zimepungua kutoka 999 mwaka 2016 hadi kufikia 729 mwaka 2018.

Jaji Mkuu ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni nakala za hukumu za kesi zimeendelea kupatikana kwa wakati na kusisitiza wahusika kuendelea kutoa kwa wakati nakala hizo na bila malipo.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma, ifikapo mwezi Juni mwaka huu zaidi ya majengo Hamsini ya mahakama yatakua yamejengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli mbiu ya siku ya sheria nchini kwa mwaka huu ni Kutoa haki kwa wakati, wajibu wa mahakama na wadau.