Guterres azungumzia mgogoro wa Venezuela

0
996

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa  umoja huo hautajihusisha na jitihada zozote zenye lengo la kumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Venezuela.

Amewaambia Waandishi wa habari jijini New York nchini Marekani kuwa hatua hiyo si kwa nia mbaya, bali ni kuepuka kuonyesha upendeleo kati ya pande zinazovutana katika mgogoro huo.

Hata hivyo Guterres amesema kuwa Umoja wa Mataifa unaufuatilia mgogoro huo wa kisiasa nchini Venezuela kwa karibu kwa kuwa unaleta wasiwasi mkubwa.

Mataifa ya Mexico na Uruguay ambayo hayajatangaza kumtambua  Juan Guaido kama Rais wa mpito wa Venezuela yalikuwa na matarajio kwamba Guterres atashiriki katika mazungumzo yanayofanyika hii leo ambayo yana lengo la kunusuru hali ilivyo sasa nchini Venezuela.

Pamoja na mambo mengine, Wajumbe wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo walitarajiwa kuhamasisha kufanyika kwa majadiliano baina ya Guaido aliyejitangaza Rais wa Mpito wa Venezuela na Rais  wa sasa wa nchi hiyo Nicolas Maduro ili kuiondoa nchi hiyo kwenye mgogoro huo wa kisiasa.