Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na Idara ya Mahakama nchini ili kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria, wiki ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza jijini humo baada ya serikali kuhamishia Makao Makuu yake.
Amesema kuwa serikali inafuatilia kwa karibu na kuzitatua changamoto zote zinazoikabili Idara ya Mahakama nchini, lengo likiwa ni kuhakikisha Wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma za kisheria.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Wiki ya Sheria ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini, hivyo ni vema ikatumika vizuri ili kufanikisha lengo la Idara ya Mahakama nchini la kumpatia haki kila mwananchi bila ubaguzi.
Ametoa wito kwa wataalamu wa masuala ya sheria nchini kutenga muda wao wa kuwasaidia Wananchi kufahamu masuala ya kisheria kwa kuwa wengi wao wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo, jambo linalochangia baadhi yao kukosa ama kupoteza haki zao.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma amesema kuwa kwa kipindi cha wiki nzima, maonesho ya Wiki ya Sheria yatafanyika jijini Dodoma na kwenye Mahakama zote kuanzia ngazi ya wilaya.
Amesema kuwa kupitia maonesho hayo, wananchi wengi watapata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali na kupata elimu kuhusu masuala ya sheria.
Kila mwaka, Idara ya Mahakama nchini imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Sheria ambayo pamoja na mambo mengine hutoa fursa kwa Wananchi kupata elimu kuhusu masuala ya sheria.