Pellegrini amuelezea Klopp

0
902

Kocha wa West Ham United, – Manuel Pellegrini amesema kuwa kocha wa Liverpool, – Jurgen Klopp amezoea kushinda kwa mabao ya Offside, kauli aliyoitoa baada ya timu yake kutoka sare ya bao moja kwa moja na vinara hao wa Ligi Kuu ya England.

Sadio Mane alianza kuiandikia Liverpool bao la kuongoza katika dakika ya 22,  bao ambalo Pellegrini amesema kuwa James Milner alikuwa katika eneo la kuotea kabla ya kutoa pasi ya kufunga kwa Mane lakini mwamuzi msaidizi hakunyanyua kibendera, kabla ya Michail Antonio kuisawazishia West Ham katika dakika ya 28 akitumia vyema makosa ya safu ya ulinzi ya Liverpool.

Baada ya mchezo huo Pellegrini akakumbushia tukio la miaka Sita iliyopita ambapo Klopp akiwa kocha wa Borussia Dortmund waliinyuka Malaga iliyokuwa ikinolewa na Pellegrini mabao  matatu kwa mawili kwenye mchezo wa robo fainali ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya ambapo mabao mawili ya Dortmund katika dakika za mwisho yalikuwa ya Offside.

Pellegrini amesema kuwa kwenye mchezo huo wachezaji wanne wa Dortmund walikuwa katika eneo la kuotea umbali wa mita saba peke yao, lakini mwamuzi akakubali goli kitendo kilichojirudia kwenye mchezo wa siku ya Jumatatu dhidi ya Liverpool,  hivyo kocha Jorgen Klopp amezoa kushinda kwa mabao ya Offside.

Kwa upande wake Klopp amesema kuwa maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo Kevi Friend kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na waamuzi wasaidizi, kwani hata yeye alisikia kuwa bao lao la kuongoza lilikuwa Offside lakini mwamuzi wa pembeni hakuashiria chochote zaidi ya kulikubali.

Kwa matokeo hayo,  Liverpool wanaendelea kusalia kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England wakifikisha alama 62 ikiwa ni alama Tatu tofauti na Manchester City walio na alama 59 katika nafasi ya pili na nafasi ya Tatu wapo Tottenham Hotspur wenye alama 57.