Zoezi la upigaji kura Kenya lakamilika

0
203

Zoezi la kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Kenya limehitimishwa rasmi saa 11 kamili jioni hii.

Vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa saa 12 asubuhi, ambapo idadi kubwa ya watu wamejitokeza kupiga kura.

Maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC)
wamesema, licha ya muda kumalizika, wananchi waliopanga mistari wataendelea kupiga kura mpaka watakapomalizika.

Jumla ya nafasi 1,882 zikiwemo za Urais, Ugavana na Uwakilishi zinagombewa katika uchaguzi huo.

Kwa kiti cha Urais, wagombea wanne wameshiriki katika kinyang’anyiro hicho huku upinzani mkubwa ukiwa kati ya Raila Odinga kutoka muungano wa Azimio la Umoja na William Ruto kutoka muungano wa Kenya Kwanza na Naibu Rais wa nchi hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye anamaliza muda wake alipiga kura katika eneo la Gatundu South na kuwasihi wananchi wapige kura na kurejea majumbani kusubiri matokeo.

Kwenye baadhi ya maeneo kulikuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja kuchelewa kwa karatasi za kupigia kura ambapo maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Kenya wamesema watafidia muda uliopotea.