Mwanafunzi afutiwa deni la milioni 9

0
246

Wizara ya Afya imemfutia deni la shilingi milioni tisa mwanafunzi Lightnes Shurima, ambalo alikua akidaiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila) kutokana na matibabu ya Baba yake (kwa sasa marehemu) aliyekua anatibiwa hospitalini hapo.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amemtaka Lightnes ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) Hombolo mkoani Dodoma kufika hospitalini hapo kesho Agosti 9, 2022 na kuonana na Mkurugenzi wa hospitali hiyo ili kuchukua kitambulisho chake.

Waziri Ummy Mwalimu amesema serikali inatambua kuwa kuna wananchi wengi ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu, hasa katika kipindi hiki ambacho matibabu yana gharama kubwa.

Pia amerudia kuzitaka hospitali zote za serikali nchini kuzingatia maelekezo ya wizara ya Afya kuwa kila baada ya siku chache zinaprint bili ya mgonjwa (mteja) ili ndugu waweze kulipia na hiyo itasaidia kuwapunguzia mzigo wa kulipa bili kubwa za matibabu kwa wagonjwa wao.

Hivi karibuni iliripotiwa kuwa Lightness Shirima anadaiwa shilingi milioni tisa, deni ambalo aliliacha baba yake aliyefariki dunia katika hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila) na yeye kuacha kitambulisho cha NIDA kama dhamana.