Rais Samia : Ongezeni kasi kwenye ukusanyaji wa kodi

0
173

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri na kuziba mianya yote ya upotevu ili miradi iliyoombwa na watendaji iweze kutekelezeka katika maeneo yote nchini.

Rais Samia ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa John Mwakangale uliopo Kyela mkoani Mbeya huku pia akiwakumbusha wananchi kuwa wazalendo kwa kulipa kodi kwa kila bidhaa wanayonunua.

“Kama kuna tozo halali iliyowekwa na serikali nenda kalipe, ili kutekeleza shughuli zetu za maendeleo”-amesema Rais Samia

Katika hatua nyingine Rais Samia ameupongeza mkoa wa Mbeya kwa kukusanya kodi vizuri kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ingawa wameshaweka bajeti tayari na kuwasisitiza wayapitie tena malengo kwani wanaweza kukusanya zaidi

“Nichukue fursa hii kuupongeza mkoa wa Mbeya, wilaya zote zimekusanya zaidi ya asilimia mia. Ingawa mmeshaweka makisio tayari naomba mpitie tena mnaweza kukusanya zaidi ya haya”-ameongeza Rais Samia.

Kuhusu Ujenzi wa Barabara ya Tanzania-Zambia (TAZAM) Rais amesema wamekubaliana kwa nchi mbili ya Tanzania na Zambia kuanza kufanyia kazi ujenzi wa barabara hiyo na kuhakikisha inajengwa kisasa.