Urusi yakosoa Spika wa Marekani kuzuru Taiwan

0
214

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergie Lavrov amesema ziara ya Spika wa Marekani kwenda Taiwan inaonesha majigambo ya Marekani kwamba inaweza kufanya chochote inachotaka.

Lavrov ameongeza kuwa kitendo hicho hakina tofauti na uhusiano wa Marekani na Ukraine kwenye vita vinavyoendelea kati yake na Urusi.

Uhusiano wa Urusi na China umeonekana kuimarika siku za usoni, ambapo China inaiunga Urusi mkono katika kudhibiti kupanuka zaidi kwa NATO, na licha ya kuwa China haijaiunga Urusi mkono kwa uwazi katika vita inayoendelea, pia haijaikosoa.

Spika wa Marekani, Nancy Pelosi aliwasili Taiwan jana licha ya kuwepo onyo kwa China kwamba kufanya hivyo ni kuingilia mambo ya ndani, na kwamba ziara hiyo itakuwa na madhara katika uhusiano wa China na Marekani.

China inashikilia kwamba Taiwan ni sehemu ya eneo lake na kwamba ni lazima ilirejeshe, huku Taiwan ikidai kwamba ni nchi huru, na sio sehemu ya China.

Umoja wa Mataifa (UN) hauitambui Taiwan kama nchi huru, lakini zipo nchi zaidi ya 10 zinazoitambua Taiwan kama nchi huru, na nchi hizo hazina uhusiano na China.