Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema kwamba wawakilishi wa Rais hawapaswi kulala, kama ambavyo Rais alisema halali, ili wahakikishe wanafikisha maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza na TBC mapema leo kuhusu maonesho ya Sikukuu ya Wakulima yanayoendelea mkoani Mbeya, Homera amesema mkoa huo umejipanga kuendelea kuzalisha chakula zaidi kulisha Tanzania yote.
“Kama alivyosemma, yeye halali, na sisi hatulali. Atakayelala kwa kweli atakuta mkeka umechanika,” amesema Homera, akiongeza kuwa atakayelala akiamka, ataamka na mkeka.
Aidha, amesema Nane Nane mkoani humo ni miongoni mwa maonesho yaliyofanya vizuri zaidi, ambao kumekuwa na bidhaa na vitu mbalimbali vya kuonesha na kutolea mafunzo ambayo wanaamini vitakuza uelewa na ujuzi miongoni mwa washiriki.
Amepongeza juhudi za serikali kuendelea kuboresha kilimo kwa kutoa pembejeo, kuhakikisha uwepo wa masoko ya mazao ya wakulima, ujenzi wa miundombinu, ikiwemo barabara na elimu kwa wakulima, kwamba vyote vinawezesha kuongeza uzalishaji.