EU Yaahidi Ushirikiano na Mahakama ya Tanzania

0
169

Umoja wa Ulaya (EU) umeahidi kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali, lengo likiwa ni kuboresha huduma za utoaji haki.

Ahadi hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na balozi EU nchini Manfredo Fanti, alipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma katika Mahakama ya Rufani kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya utoaji haki nchini.

Amesema mazungumzo yake na Jaji Mkuu yamelenga kuangalia na kubaini maeneo yenye changamoto yanayohitaji ushirikiano, ili changamoto hizo zishughulikiwe.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amemueleza Balozi huyo kuwa, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Ameongeza kuwa miongoni mwa vipaumbele ambavyo Mahakama inasisitiza katika kuangalia njia za haraka zaidi zitakazosaidia kupunguza mlundikano wa mashauri ni kutumia usuluhishi na kuanzisha mahakama ndogo zitakazosaidia kusikiliza na kuamua mashauri ya kibiashara.

Jaji Mkuu amesema, bado kuna changamoto kadhaa ambazo Mahakama inakabiliana nazo, ikiwemo namna ya kufikisha huduma za utoaji haki kwa wananchi.