Ajinyonga baada ya kumnyonga Mkewe

0
181

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Tanga, Emmanuel Jerome (32), anadaiwa kumnyonga mke wake, Lucy Nshoma (34), katika nyumba ya kulala wageni mkoani Rukwa, kisha na yeye kujinyonga kwa kutumia kamba juu ya mti siku moja baadaye mkoani Katavi.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame amesema marehemu ni mkazi wa Tanga na chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi.

Kamanda Makame amesema marehemu Jerome alikua na mgogoro na mke wake, ambapo alimtuhumu kutoka kimapenzi na wanaume wengine.

Amesema Jerome na mkewe walipanga safari kuelekea mkoani Rukwa, ambapo ni nyumbani kwao mke wake na walifikia nyumba ya kulala wageni Julai 26, 2022, ndipo usiku alipochukua uamuzi wa kumnyonga mkewe.

RPC Makame, ameeleza kuwa baada ya kufanya tukio hilo mkoani Rukwa alikimbilia mkoani Katavi na Julai 27,2022 usiku, eneo la mtaa wa Ilembo, Manispaa ya Mpanda, alichukua uamuzi wa kujinyonga na walikuta mwili wake ukiwa unaning’inia kwenye kamba.