Kagera ipo imara kulinda bomba la mafuta

0
143

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amesema, mkoa huo umejipanga kuulinda mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.

Meja Jenerali Mbuge amesema hayo wakati wa mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mkoani Kagera, ambapo amezungumzia ujio wa mradi wa bomba hilo nchini ukitokea Uganda.

Amesema mkoa wa Kagera hauna viwanda vingi, hivyo ujio wa mradi huo wa bomba la mafuta ghafi na kupita mkoani humo utaleta chachu ya kukua kwa uchumi wa mkoa na maendeleo ya wananchi wake.

“Niwahamasishe wananchi wa Tanzania hasa wa mkoa wa Kagera kuchangamkia fursa za mradi huu ambao umekuja muda muafaka na Serikali inausimamia kwa ukaribu sana, ili kuleta faida kwa Taifa.” ameongeza Meja Jenerali Mbuge

Huo ni mradi wa kimkakati wa Serikali lupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na unatarajiwa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania.

Dola bilioni 5.1 za kimarekani ambazo ni sawa na shilingi takribani trilioni 11 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.