Rais Samia : Tutaendelea kuboresha miundombinu

0
142

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendelea kuboresha miundombinu ya Afrika Mashariki, ili uchumi wa nchi zilizopo katika ukanda huo uendelee kukua.

Rais Samia amesema hayo mkoani Arusha wakati wa ufunguzi wa barabara ya mchepuko ‘Bypass’ inayounganisha Arusha na Taveta hadi Voi nchini Kenya, yenye urefu wa kilomita 42.4 ambayo ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 197.

Amesema Tanzania inaenda kuunganisha Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa njia ya reli ya kisasa (SGR), ambayo ujenzi wake unaendelea.

“Hatutaishia kwenye barabara pekee, tutaunganisha mataifa haya kwa njia ya reli na hata maziwa makuu ili uchumi uweze kupiga hatua zaidi.” amesema Rais Samia

Kwa upande wake Rais wa Kenya ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta amesema, mataifa hayo mawili yana ushirikiano wa muda mrefu na kupitia barabara hiyo Wakenya watauza bidhaa Tanzania na Tanzania kuuza bidhaa Kenya.

Uhuru Kenyatta- Rais wa Kenya

Barabara hiyo ya mchepuko ‘Bypass’ inasimamiwa na Wakala wa Barabarani Tanzania (TANROADS).