Viongozi wanaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha, kujadili utekelezaji wa soko la pamoja baina ya nchi hizo ikiwemo kuangazia mafanikio, fursa zilizopo, changamoto na namna watakavyoendeleza ushirikiano.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema, ni muhimu kwa mataifa wanachama kutumia rasilimali zilizopo kwa kuzalisha zaidi na kufungua viwanda kwa ajili ya kuchakata malighafi na kutumia wenyewe bidhaa kuliko kusafirisha na baadae zinanunuliwa.
“Afrika kwa ujumla imebarikiwa kwa vitu vingi, ni lazima tujiendeleze wenywe, tuwapeleke watoto wetu shule, tutumie rasilimali zetu wenyewe, hiyo ndio silaha pekee ya kufikia maendeleo na soko kupanuka zaidi.” amesema Rais Kenyatta
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo amesema, ni muhimu kuangalia kwa makini miundombinu iliyopo maeneo yanayozalisha kwa wingi, ili iwe rahisi kusafirisha bidhaa kwa walengwa.
Naye Rais wa Yoweri Museveni wa Uganda amesema, kutokuwa na mikakati sahihi ni miongoni mwa chanzo cha kutokuwa na maendeleo.
“Mnaona Bara la Amerika wana kila kitu lakini kila siku unasikia watu wao wamekimbilia Ulaya kwa sababu ya umaskini, hii inatokana na kutokuwa na mikakati sahihi ya kutumia rasilimali zilizopo kule.” amesema Rais Museveni
Viongozi wengine waliopata nafasi ya kuchangia hoja ya namna ya kuboresha soko la pamoja ni Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi, mwakilishi wa Rais wa Sudan Kusini Barnaba Marioo Benjamin, mwakilishi wa Rais wa Rwanda ambaye ni Waziri Mkuu wa nchi hiyo Édouard Ngirente na mwakilishi wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye ni Waziri Mkuu Jean-Michel Sama Lukonde.
Mkutano huo unafanyika kwa muda wa siku mbili na utahitimishwa Julai 22, 2022 huku ajenda kuu ikiwa ni kuendeleza ushirikiano baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.