Benki ya Dunia kwa kushirikiana na washirika wake imeahidi kusaidia juhudi za serikali za kufanikisha mapinduzi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kutoa fedha pamoja na ushauri wa kitaalam.
Ahadi hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini Mashariki, Victoria Kwakwa alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba.
Amesema janga la UVIKO-19 na vita vinavyoendelea baina ya Russia na Ukraine vimeibua changamoto kubwa ya uhaba wa mazao ya nafaka, na kwamba Tanzania ikijipanga vizuri inaweza kuwa ghala la chakula na kuifanya ijitosheleze kwa chakula na kutoagiza chakula kutoka nje.
Benki ya Dunia pia imeipongeza Tanzania kwa kuamua kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye maeneo ya uzalishaji kikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi mambo ambayo yatachochea ukuaji wa kipato cha wananchi na kukuza uchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema serikali imeamua kuwekeza fedha kwenye maeneo ya uzalishaji akitolea mfano wa ongezeko la bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 200 hadi zaidi ya shilingi bilioni 900 ili kuiwezesha sekta hiyo kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuzalisha ajira kwa wananchi.
Ameishukuru Benki ya Dunia kwa uwekezaji wa dola bilioni 2.8 za Kimarekani kwenye miradi 11 ya kimkakati iliyowasilishwa katika Benki hiyo.