Mwili wa Dos Santos kufanyiwa uchunguzi

0
177

Mahakama nchini Hispania imeamuru kufanyiwa uchuguzi mwili wa Rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo Dos Santos, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika hospitali moja iliyopo kwenye mji wa Barcelona.

Amri ya kufanyiwa uchunguzi mwili wa Dos Santos imetolewa na mahakama hiyo, kufuatia shutuma zilizotolewa na upande wa familia kuwa kulikua na mpango wa kumuua.

Ombi la kutaka mwili wa Jose Eduardo Dos Santos ufanyiwe uchunguzi liliwasilishwa mahakamani hapo na binti yake, Tchize Dos Santos.

Akiwasilisha ombi hilo Tchize alisema mahasimu wa kisiasa wa baba yake walikuwa hawataki ausaidie upinzani katika uchaguzi mkuu ujao.

Nao mawakili wa familia ya Dos Santos wamepinga mpango wa serikali ya Angola kusafirisha mwili wa kiongozi huyo kwenda nchini humo kwa ajili ya mazishi, huku wakidai mwenyewe alitaka azikiwe kwa siri nchini Hispania.

Wamesema aliamua azikwe Hispania kwa kuwa alikuwa na wasiwasi huenda masuala ya kisiasa yataingizwa kwenye msiba wake, na hivyo kusababisha watoto wake washindwe kuhudhuria mazishi yake na pia watashindwa kusafiri kwenda nchini humo kuona kaburi.

Naye Rais João Lourenço wa Angola, mtu ambaye alichaguliwa na Dos Santos kuwa mrithi wake na ambaye wote walikuwa wanatoka chama tawala cha MPLA, amekanusha serikali yake kujihusisha na kifo cha kiongozi huyo.

Amesema serikali ya Angola ina wajibu wa kuandaa mazishi ya Dos Santos kwani alikuwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo na alikuwa na mchango mkubwa, na kuongeza kuwa raia yeyote wa nchi hiyo atakayetaka kushiriki katika mazishi ya kiongozi huyo ruksa kufanya hivyo.

Jose Eduardo Dos Santos ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79. amekuwa akipatiwa matibabu nchini Hispania tangu alipohamia nchini humo baada ya kuondoka madarakani nchini Angola mwaka 2017.

Aliiongoza Angola kwa takribani miaka 38 kuanzia mwaka 1979 hadi mwaka 2017, na amefariki dunia baada ya kupata shambulio la moyo.

Dos Santos alichukua madaraka nchini Angola baada ya kufariki dunia kwa kiongozi aliyeongoza mapambano ya uhuru nchini humo, Agostinho Neto.