Mzee Rehani Waikela azikwa

0
152

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ((CCM) Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, ameungana na mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele kuunga mkono harakati za uhuru wa Tanganyika Mzee Rehani Bilal Waikela aliyefariki dunia leo na kuzikwa leo mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza katika ibada ya sala ya maiti iliyofanyika kwenye msikiti wa Kichangani Magomeni, Shaka amesema Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia Suluhu Hassan amemtaja Mzee Waikela kuwa ni mzalendo, jasiri mwenye uthubutu na mtu aliyejitolea kwa hali na mali katika kupigania Uhuru wa Tanganyika.

Katika salamu zake zilizowasilishwa wakati wa mazishi hayo na Shaka, Rais Samia Suluhu Hassan amesema “Tumempoteza miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele katika kufanikisha uhuru wa Tangayika kwa sababu alikuwa jasiri, mzalendo mwenye uthubutu na utayari wa kujitolea nguvu na rasilimali zake wakati wa mapambano ya kutafuta uhuru, mchango wake ni mkubwa ambao chama na serikali tunauthamini na tutaukumbuka.”

Mzee Rehani Bilali Mwaikela amezikwa katika makaburi ya Mwinyimkuu, wilaya ya Kinondoni mkoani Dar ss Salaam.